Mabadiliko ya wapenzi yaliyogusa nyoyo za wengi Kenya
Kwa wengi, mwezi wa Februari ambao kawaida umekuwa ukihusishwa na mapenzi unakaribia kufikia ukingoni, na wengi wameanza kuisahau Siku ya Wapendanao. Kwa Samuel Githae na Zipporah Njeri, siku hii maarufu kwa upendo ilikuwa mwanzo wa matukio ambayo yamechangia kuinuliwa kwao kutoka kwa maisha ya kutotambuliwa mjini hadi kuwa watu mashuhuri. Wamekuwa bila makao rasmi, wakilala barabarani, kwenye vituo vya filamu na wakati mwingine katika nyumba za marafiki zao. Lakini sasa watahamia katika nyumba mpya rasmi Jumamosi, ambayo wamelipiwa kodi na mhisani. Isitoshe, wataabiri ndege kwa mara ya kwanza kwenda likizoni katika hoteli moja ya ufukweni pwani ya Kenya wiki ijayo. "Siamini kwamba nitapanda ndege," Njeri aliambia BBC, akionekana mwenye furaha, akipigapiga mikono kama ndege anayejiandaa kupaa. Yote yalianza kutokana na wazo la mpiga picha Johnson Muchiri kutoka kwa kampuni ya Muchiri Frames, na wafanyakazi wenzake, kutaka kufanya jambo la kipekee. Jacinta N...