"Tumemchukulia hatua tayari" - Muliro
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Muliro J. Muliro amefunguka na kusema kuwa wamemchukulia hatua za kinidhamu askari polisi wake mmoja ambaye jina lake halijawekwa wazi kufuatia kuonekana akichukua rushwa kwenye video za mitandaoni. Hatua hiyo ya jeshi la polisi imekuja masaa kadhaa baada ya Mwanaharakati wa mambo ya siasa mtandaoni, mrembo Mange Kimambi kuposti video ya askari polisi akichukua rushwa ya pesa kutoka kwa raia ambaye alitenda kosa la barabarani. Akithibitisha juu ya kuchukua za kinidhamu kwa askari huyo Kamanda Muliro amesema ni kweli Jeshi la Polisi limechukua maamuzi hayo kwa askari huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake. "Ni kweli tumechukua hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria na kanuni za kipolisi kwa askari yule, kuhusu jina lake kwa sasa hatuwezi kuliweka wazi kwa kuwa jeshi la polisi haliwezi kufanya kazi kwa matangazo" alisema Muliro