Ujumbe wa Kwaresima 2018 kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu ndiyo kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa mwaka 2018. Ni ujumbe unaozingatia matukio makuu matatu: Jubilei ya Miaka 150 ya Ukristo Tanzania Bara, Miaka 50 ya Tamko la Maaskofu kuhusu Mwelekeo na Hatima ya Tanzania na Maandalizi ya Uchaguzi wa viongozi wa Serikali za mitaa utakaofanyika mwaka 2019. Wapendwa Familia ya Mungu, Na Watu Wote wenye Mapenzi Mema, “Neema na iwe kwenu, na amani zitokazo kwa Mungu, Baba yetu” (Kol 1:2).
Utangulizi
Kama ilivyo ada ya Wakristo pote ulimwenguni, kwa kipindi cha siku arobaini kabla ya kuadhimisha Jumapili ya Ufufuko wa Bwana Wetu Yesu Kristo, Wakristo hutumia muda huo kufunga, kufanya toba na kufanya matendo ya huruma kwa wote wenye mahitaji huku wakijitafakari kuhusu uhalisia wa hali yao ya kuwa ni wenye dhambi mbele ya Mungu, ili waweze kufanya toba ya kweli na yenye mageuzi na wongofu katika maisha. Mwaka huu kipindi hiki, kijulikanacho kama kipindi cha Kwaresima, kinaanzia tarehe 14 Februari Jumatano, siku ambayo inajulikana kwa jina la Jumatano ya Majivu, mpaka tarehe 29 Machi, ambayo itakuwa ni siku ya Alhamisi Kuu.
Kwa mwaka huu wa 2018 kipindi hiki, cha kujitafakari mbele ya Mungu na kufanya toba hususan uhai wa imani yetu kwa njia ya matendo ya huruma, haki, upendo na amani kwa jirani zetu, ni kipindi chenye upekee wa aina yake kwa sababu kuu tatu: 1) Ni katika mwaka huu ambapo Kanisa Katoliki Tanzania linaadhimisha na kusherehekea miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara, na kilele chake kitakuwa tarehe 2 Oktoba; 2) Mwaka huu pia utakuwa ni mwaka wa 50 tangu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania watoe tamko rasmi kuhusu mwelekeo na hatima ya nchi yetu; na 3) Mwaka huu ni mwaka wa maandalizi ya utekelezaji wa haki ya msingi ya kidemokrasia ya raia wote ya kuchagua viongozi wa serikali zetu za mitaa, vijiji na vitongoji hapo mwakani 2019. Kwa sababu kuu hizo tatu, ni vema tafakari yetu ya Kwaresima ikalenga katika swali ambalo, kwa namna moja au nyingine, linahusu sababu hizo tatu. Kwa njia ya swali hilo mwanadamu hudiriki kumhoji na kumuuliza Mungu na Muumba wake kuhusu hali ya binadamu mwenzake. Swali hilo ni “Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” (Mw. 4:9).
Hali halisi ya nchi yetu, kwa yeyote anayesoma ishara za nyakati kwa makini, inalifanya swali hilo liwe na uzito wake kuendana na sababu hizo kuu tatu zilizotolewa. Lakini pia, tukumbuke kuwa mwaka 2018 ni mwaka wa sabini (70) tangu Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa walipotamka rasmi na kujifunga kuhakikisha kuwa Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamula mwaka 1948 linatekelezwa. Na sasa tuone ni kwa namna gani swali hilo linatuhusu kwa kuangalia misingi ya sababu hizo kuu tatu.
Kuhusu sababu ya kwanza, ni lazima tunapoadhimisha miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara tujiulize hilo swali kwa namna ifuatayo: “Je, sisi Wakatoliki katika kipindi hicho cha miaka 150 tumekuwa walinzi wa binadamu wenzetu, ambao tumefanywa kuwa ndugu zao kama Familia ya Mungu kupitia Mwanae Yesu Kristo na Mama yetu Bikira Maria?”. Kuhusu sababu ya pili, tujiulize swali hilo hilo kama ifuatavyo: “Je, katika kipindi hicho cha miaka hamsini, kuanzia 1968 mpaka mwaka huu 2018, sisi Wakatoliki tumekuza roho na moyo wa kuwajali binadamu kama ndugu zetu, kuendana na barua ya kichungaji ya mwaka huo, yenye kichwa cha habari The Church and Developing Society of Tanzania, iliyotuasa kuwa falsafa na imani ya Azimio la Arusha, Azimio ambalo lilitoa mwelekeo na hatima ya nchi yetu, inakubaliana kwa karibu kabisa na ( kwa kunukuu sehemu ya ujumbe huo) “roho ya kweli ya Kristo na Kanisa, roho ambayo ni ya udugu, ya kumegeana, ya kuhudumiana na ya kufanya kazi kwa bidii?” Kwa kusisitiza ukaribu huo kati ya Azimio la Arusha na roho ya kweli ya Kikristo, barua hiyo ya kichungaji ilizingatia barua ya Yakobo, 2:14-17 inayosema kuwa imani bila matendo ni imani mfu!
Kuhusu sababu ya tatu, baada ya kufanya toba na kusherehekea Ufufuko wa Bwana Wetu Yesu Kristo, tukiwa na ari na mwelekeo mpya wa maisha ya Kikristo yanayodhirishwa na imani hai, swali hilo tulihusishe na dhamira ya kweli ya viongozi wetu watarajiwa wa serikali za mitaa, kwa kujiuliza, “Mwaka huu wa maandalizi ya kuchagua viongozi wa serikali zetu za mitaa, vijiji na vitongoji, tufanye nini ili maandalizi yetu ya uchaguzi yatupe viongozi wetu wa karibu ambao hawatakwepa wajibu wao kwa kujitetea kwa mtazamo wa swali kama hilo?” Hivyo basi, ili kuhakisha kuwa tuna pata majibu ya kweli na yenye kuleta mabadiliko katika nafsi zetu na mahusiano na mashirikiano katika jamii yetu, ujumbe huu wa Kwaresima una lengo la kuwahimiza, kuwahamasisha na hata kuwadai waumini Wakatoliki wote kuuitikia kwa moyo wa toba, mageuzi na kushiriki kwa kujitoa zaidi katika uinjilishaji wa nchi yetu kama mwanga na chumvi ya ulimwengu wa Tanzania.
Kufikia lengo hilo, tunahimiza Jumuiya Ndogondogo katika kila parokia ziutafakari kwa makini ujumbe huu, zipange namna ya kuutekeleza kwa kuzingatia hayo maswali matatu. Ili kufanikisha hilo, tunatoa mwongozo ufuatao katika hatua tatu: 1) Kusoma ishara za nyakati za Tanzania na kuzichambua; 2) Kuzitathmini ishara hizo kwa misingi ya Injili na tunu za Ufalme wa Mungu kuendana na masomo na Injili ya Jumatano ya Majivu; na 3) Kufanya maamuzi yatokanayo na tathmini hiyo na kupanga utekelezaji wa maamuzi hayo. Tunawaalika basi, tutembee pamoja katika kulitafakari fumbo la imani yetu, huku tukiomba neema ya Mungu ifanye kazi ndani yetu na kutujalia kukua katika kumpenda, kumjua na kumtumikia Mungu na vivyo hivyo kumpenda jirani huku tukitumikiana sisi kwa sisi.
SURA YA KWANZA: BASI ENENDENI
Wamisionari waliokuja kuinjilisha Tanzania ya sasa walifika Zanzibar mwaka 1860 wakitokea jimbo la Reunion. Miaka minane baadae, Wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu, wakisukumwa na shauku ya kuinjilisha maeneo mapana zaidi, walisafiri kutoka Zanzibar na kutia nanga katika mji wa Bagamoyo mnamo mwaka 1868, ambapo walianzisha jumuiya ya kwanza ya wakristo ambao wengi wao wakiwa ni wale waliokombolewa kutoka utumwani. Hivi jumuiya hii ya kwanza ya Wakristo ikawa na sifa ya kukombolewa, si tu kiimani, bali hata kijamii. Hawa walifanywa kuwa watu huru kiroho, kimwili na kiutu. Mwanzo huu wa imani Zanzibar na Bagamoyo umekuwa mlango wa imani kwa maeneo yote ya ukanda huu wa Maziwa Makuu. Kwa upande wao, Wamisionari wa Afrika wlijielekeza maeneo ya Magaharibi ya Tanganyika na kuvuka maziwa yote makuu. Nao Wamisionari Wabenediktini, baadaye, walielekea maeneo ya Kusini mwa Tanganyika. Makundi haya matatu yalifuatiwa na wamisionari wa Mashirika mengine waliosambaa maeneo mbalimbali ya tanganyika.
Roho ya umisionari
Kanisa kwa asili yake ni la kimisionari. Umisionari ndiyo mtima wa Kanisa, na mmisionari hajitumi bali anatumwa. Mmisionari wa kwanza ni Bwana Wetu Yesu Kristo. “Kama vile Baba alivyonituma mimi, nami nawatuma ninyi” (Yn 20:21). Kisha wale wote waliomvaa Kristo kwa Ubatizo nao kwa muda wao, hali zao na mazingira yao wanatumwa kuendeleza utume wa Kristo. Wanatumwa kuujenga Ufalme wa Mungu. Anayetumwa hapeleki ujumbe wake, haendi kujihubiri mwenyewe, bali anapeleka ujumbe wa yule anayemtuma. Ujumbe unaobeba utume wetu uko wazi: “Enendeni basi, mkawafanye watu wa mataifa yote wawe wanafunzi wangu” (Mt 28:19). Sisi tulimpokea Kristo na kufanyika kuwa wanafunzi wake tunatumwa kuwafanya mataifa yote pia kuwa wanafunzi wake. Bwana Yesu anayetutuma anatuelekeza ni kwa namna gani tunaweza kuutekeleza wajibu na utume huo mkubwa: “Mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu. Wafundisheni kuyashika maagizo yote niliyowapeni” (Mt 28:19b-20).
Sadaka ya umisionari
Umisionari ni kutoka: “Enendeni basi”. Bwana wetu Yesu Kristo hakuwaambia mitume wake wakae wangojee watu waje. Hapana. Tokeni mkakutane wa watu walipo. Tendo la kutoka katika mazingira tuliyozoea, hali, maisha na usalama tulionao inadai kuwa tayari kutoa sadaka. Wamisionari waliokuja kwetu waliacha yote: jamaa, mali, usalama, raha, n.k.; wakaja kukabiliana na adha, magonjwa, hatari na hata kifo kilichotokana na maradhi ya nchi za ukanda wa joto (tropikali), kushambuliwa na wanyama na hata kushambuliwa na maharamia. Walitoa sadaka kubwa.
Na jambo kubwa ni kwamba walitoa sadaka hiyo kwa furaha. Ari na kiu yao ilikuwa kutekeleza agizo la Kristo: “Enendeni basi”. Walitamani kufika hata miisho ya dunia ili kuwafanya watu wamjue, wampende na wamtumikie Mungu na hivi kufanyika kuwa wanafunzi wake. Ndiyo maana hata pale ambapo wengi wao walipofariki kutokana na adha tulizoona hapo juu, bado wengine walikuja tu kwa furaha bila woga. Kwani katika kujitoa maisha yao kama sadaka walipata faraja ya ahadi ya Kristo kwa wale wote wanaoitikia mwito wa “Enendeni basi!”. Wamisionari hao waliifahamu ahadi ya Kristo na ndiyo maana hiyo ilikuwa faraja yao. Petro anapomwuliza Yesu, “Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata tutapata nini basi?” (Mt 19:27). Yesu anamjibu akitoa ahadi bora kabisa: Aliyeacha vyote kwa ajili ya jina lake, “atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele” (Mt. 19:29). Bwana Yesu anapowatuma wanafunzi wake alipokuwa anakaribia kupaa Mbinguni, aliwaambia, "… enendeni ulimwenguni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika Mimi niko pamoja nanyi sikuzote, hadi mwisho wa nyakati. Amen” (Mathayo 28:19-20).
Maneno haya ya Yesu yanaonesha upendo wa hali ya juu aliokuwa nao Mungu kwa wanadamu, kutupa nafasi ya kuwa wana wa Mungu. Kumfahamu Mungu kwa kuacha njia zetu mbaya. Yesu hakuwaambia wanafunzi wake wasubiri watu wawafuate, ili wapate kuwafundisha na kuwabatiza, lakini aliwaambia wawafuate watu walipo, na kuwafundisha juu ya Ufalme wa Mungu na kuwabatiza katika Utatu Mtakatifu, yaani Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Maagizo haya ya Yesu yalifuatwa na kwa sababu hiyo watu wote duniani tumepata kumjua Mungu wa kweli kupitia kwa Mwanae. Bahati kubwa namna gani! Yesu anatutaka wote tupate kuwa wamisionari kwa wenzetu, kwani ijapokuwa tumepata kumjua Mungu, na kuwa wakristo, yafaa kujiuliza ni mara ngapi tunamuishi Kristo? Ni mara ngapi tunaonekana kwa watu wengine wasiomjua Kristo bado kuwa sisi tu wana wa Mungu kwa pendo la kuitwa wana wa Mungu? (1 Yoh 3:1).
Mtakatifu Yohane Mwinjili katika Waraka wake wa kwanza kwa watu wote anasema: “Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo. Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu” (1Yoh 3:2-3). Ni dhahiri kila mmoja wetu anatamani na kuweka tumaini lake katika kumuona Mungu. Lakini je, mara ngapi tunamwona Mungu kupitia ndugu zetu na wale wanaotuzunguka? Je, kumuona Mungu ni Kanisani tu au hata kwenye jamii? Haya ni maswali ambayo kila mmoja wetu anapaswa kujiuliza. Kazi alizotupa Mungu ni kwa ajili ya utukufu wake. Kazi ni huduma, kwa maana unafanya kazi unayofanya ili kumsaidia mtu mwingine. Je, huyo unayemsaidia anaonja upendo wa Kristo ndani yako? Anapata kumsifu na kumshukuru Mungu kupitia wewe? Kama jibu ni hapana, basi yafaa kujitafakari kwa upya.
Umisionari ni zawadi, ni sadaka ni upendo unaozidi hali yetu ya kibinadamu. Ni kule kumpendeza Mungu na kutamani kila anayekuzunguka aonje pendo la Mungu. Umisionari wa sasa si kama ule uliokuwa miaka 150 iliyopita, ambapo kuinjilisha ilikuwa ni muhimu na lazima kwani watu hawakuwa wakimjua Mungu wa kweli. Unijilishaji ulifanikiwa, ijapokuwa kwa kukabiliana na changamoto nyingi, kwa ajili ya upendo na ujasiri wa kimungu wamisionari hawa waliokuwa nao. Uinjilishaji mpya leo hii unalenga kuwasaidia Wakristo kuuishi Ukristo kadiri ya mazingira ya leo, na kufanya hivyo kwa matendo, na hivyo kuwa kielelezo cha kweli cha imani.
SURA YA PILI: SASA NI ZAMU YETU
Mwenyeheri Paulo VI alipotembelea Uganda mwaka 1969 alilikumbusha Kanisa katika Afrika kwamba wakati umewadia wa kuwa wamisionari baina na miongoni mwetu. Akisemea jambo hilo nchini Uganda, Paulo VI alisema: “Kwa sasa, ninyi Waafrika mu wamisionari baina na miongoni mwenu. Kanisa la Kristo limekwisha pandwa vema na kwa uhakika katika udongo huu uliobarikiwa. ... Kwa maneno mengine, ninyi Waafrika lazima sasa, katika Bara hili, muendeleze ujenzi wa Kanisa.... Kanisa kwa maumbile yake daima ni Kanisa la kimisionari”. Hii ni kutaka kusema kwamba hatupaswi kudhani kuwa mmisionari ni mtu anayetoka nje ya nchi kuja kwetu. Umisionari kwa maana pana ni kumshuhudia Kristo kwa maneno na matendo yetu popote tulipo. Umisionari ni kuachana na ubinafsi, ni kukumbuka kuwa popote tulipo tunapaswa kutenda na kunena yale yanayojenga Ufalme wa Mungu na kusaidia kuwafanya watu wengi kuwa wanafunzi wa Kristo. Kristo anaposema, “Nanyi mtakuwa mashahidi wangu” (Mdo 1:8), anataka kusema kama tumemsikia, kama tumemjua, na zaidi sana kama tunampenda, basi hatuwezi kuacha kumshuhudia kwa wengine. Moto wa furaha wa kumjua Kristo utatusukuma kuhakikisha tunafanya kila tunavyoweza ili mwana wa mtu atakapokuja akute bado kuna imani duniani (Rej. Lk 18:8).
Jambo hili linadai ujasiri wa imani utokao kwa Roho Mtakatifu. Ndiyo maana Mitume wa Yesu hata walipokamatwa, kuteswa na kufungwa hawakurudi nyuma: “Hatuwezi kuacha kusema juu ya mambo yale tuliyoyaona na kuyasikia” (Mdo 4:20). Baba Mtakatifu Francisko, katika hati yake ya kichungaji Furaha ya Injili (Evangelii Gaudium, 14), anapendekeza mambo haya yafuatayo yatubidishe:
1. Kuwasaidia waamini wakue kiroho ili waweze kupokea upendo wa Mungu kwa utimilifu zaidi katika maisha yao.
2. Kuwasaidia wabatizwa ambao maisha yao hayaonyeshi wajibu wa ubatizo, ambao hawana uhusiano wa maana na Kanisa na hawapati tena faraja inayotokana na imani.
3. Umuhimu wa kuihubiri Injili kwa wale ambao bado hawamtambui Yesu Kristo au daima wamemkataa.
Hii ndiyo namna bora kabisa ya kuwa “katika hali ya umisionari daima” (EG, 25), na ndiyo namna ya kudhirisha kuwa sasa ni zamu yetu nasi kuhubiri yale tuliosikia na kuyaona. Bidii ya kufanya mambo hayo matatu yaliyotajwa na Baba Mtakatifu Fransisko itatuepusha na tabia ya Kaini ambaye hakujali wala hakuona kuwajibika juu ya mustakabari wa ndugu yake Abeli. Hivyo basi, kuwa mmisionari kunahitaji sana moyo wa kujali kabisa hatima ya wokovu ya kila binadamu kwa kumjali katika nyanja zote za maisha yake kiroho, kiakili, kimwili na kijamii. Bila ya kuwa na moyo wa kujali, tutakuwa wakatili kama Kaini alivyokuwa kwa ndugu yake Abeli!
SURA YA TATU: “MIMI NI MLINZI WA NDUGU YANGU?”
Moja ya majibu ya kukatisha tamaa kabisa katika Maandiko Matakatifu ni hili jibu la Kaini anapoulizwa na Mungu baada ya kuwa amemwua ndugu yake Abeli, “Yuko wapi Abeli ndugu yako?” (Mwa 1:9), Kaini anajibu, “Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” (Mwa 4:9b). Kaini hajali na haoni kuwajibika kwa namna yoyote juu ya mustakabari wa ndugu yake. Lakini zaidi sana, anakuwa ni kielelezo cha dhamiri iliyokufa, kwani anajua kilichotokea na hajali lolote kuhusu hali ya ndugu yake! Ni kwa mtazamo huo basi nasi tujitathmini na tuwe wa kweli kwa dhamiri zetu. Je, kama wamisionari tunaowajibika kwa ndugu zetu, tunaelezaje hali ilivyo sasa katika jamii yetu ya Tanzania? Je, tunasoma alama za nyakati zetu vema kiasi kwamba tunaguswa kama wamisionari na tunapeleka Habari Njema inayoonesha kuwa sisi ni walinzi wa ndugu zetu?
Dalili za Nyakati Zetu Tanzania
Ili kuweza kuleta mabadiliko katika nafsi zetu na katika jamii yetu, Kanisa siku zote linatufundisha, kwa busara na hekima ya Roho wa Mungu, ulazima wa kusoma ishara za nyakati ili kujua ni nini kinachoendelea katika jamii. Kuhusu nchi yetu ishara za nyakati tutaziangalia katika maeneo matatu, yaani kisiasa, kijamii na kiuchumi, kwa lengo la kujitathimini.
- Kisiasa Kikatiba, nchi yetu inafuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Katiba na Sheria mbalimbali zimeainisha utaratibu wa kazi na shughuli za vyama vya siasa. Ili kuhakikisha kwamba kazi na shughuli za vyama vya siasa zinakuwa endelevu, vyama vyenye kukidhi vigezo hupewa ruzuku kupitia Bajeti ya Serikali inayopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania. Hata hivyo, shughuli za siasa bado zinaendelea kuzuiwa kwa kutumia vyombo vya dola. Maana yake ni kwamba shughuli za kiuenezi za vyama vya siasa, kama vile mikutano ya hadhara, maandamano, makongamano, mijadala na hata mikutano ya ndani, ambayo ni haki ya kila raia, zimekoma mpaka uchaguzi mwingine. Kisheria, huu ni uvunjifu wa Katiba na Sheria za nchi.
Vile vile baadhi ya vyombo vya habari vimefungiwa au kusimamishwa kwa muda, na hivyo kupunguza uwigo wa uhuru wa wananchi wa kupata habari, maoni na wa kujieleza. Kufungiwa huku kwa vyombo vya habari kumeenda sambamba na kuminya uhuru wa Mahakama na Bunge kwa njia ya kuminya haki ya wabunge na kutowapa nafasi ya mikutano ya hadhara kama haki yao ya msingi ya Kikatiba. Katika mazingira haya ni rahisi kwa jamii kufarakana na hata kujenga chuki kiasi cha kuhatarisha amani, usalama na hadhi ya uhai wa binadamu. Kumekuwapo pia hali ya vurugu katika chaguzi mbalimbali. Chaguzi hizi zinaacha nyuma uchungu, hasira, tamaa ya kulipa kisasi na hata kususia chaguzi nyingine. Hali hii ni hatari kwa mustakabali wa Taifa letu. Tukiiachia hali hii izoeleke tushishangae huko mbeleni kujikuta katika mifarakano mikubwa zaidi itakayobomoa misingi ya amani na umoja wa kitaifa.
- Kiuchumi Hapa ni vema tukajiuliza maswali ya msingi kabisa kuhusu kujali katika maisha ya walio wanyonge ili umisionari wetu ulete nafuu katika mahitaji ya lazima kwa wale wanyonge, maskini na walio pembezoni mwa jamii. Hebu tujiulize:
- Tunazitumuaje mali na rasilimali nyingine tulizokabidhiwa na Mungu kama mawakili wake?
- Tunalipa kodi stahiki kwa ajili ya kugharamia huduma za jamii ambazo serikali inapaswa kutoa kwa ajili ya wananchi?
- Wale ambao tu waajiri, tunawajali wafanyakazi na wahudumu wetu kwa kuwalipa mishahara ya halali?
- Wale ambao tu wafanya biashara, tunalipa kodi zote kihalali?
- Wale ambao tumepewa jukumu la kukusanya kodi, ushuru na ada nyingine tunafanya hivyo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu husika?
- Tunaepukanaje na kishawishi cha rushwa, hongo, mulungula, magendo au aina yoyote ya ufisadi?
- Kijamii
Sasa hivi bado kuna kishawishi cha kupingana na azma ya kuboresha maisha ya kijamii. Hii inajidhihirisha kwa njia ya uhasama, ugomvi, ukatili kwa watoto na wanawake, ujambazi, na maovu mengine kiama hayo miongoni mwa jamii yetu. Kama wamisionari tunaopaswa kuleta habari njema kwa ndugu zetu, kwa nini turuhusu roho ya namna hii ambayo kwa kweli ni roho ya Kaini inayouliza kwa jeuri kabisa: ‘Mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?’
SURA YA NNE: NIMRUDISHIE BWANA NINI?
Alama za nyakati katika jamii yetu ya leo, na tafakari kuhusu maswali yaliyoulizwa havina budi kutupa msukumo ambao ni kinyume kabisa na mtazamo wa Kaini. Msukumo huo ni ule unaoanzishwa na kutambua mema aliyotufanyia Mungu Baba, hasa lile jema kuu la kuletewa, kuikubali na kuiishi Injili ya Bwana Wetu Yesu Kristo kama wamisionari wake waaminifu. Na moyo huu unasimama juu ya swali “Nimrudishie nini Bwana kwa mema aliyonitendea?” (Zab. 116:12) Neno la Bwana Mungu wetu na Baba wa Mkombozi wetu Yesu Kristo, kama linavyosomwa siku ya Jumatano ya Majivu, siku tunapoanza kipindi cha Kwarezima, lina msukumo huohuo! Masomo pamoja na Injili ya siku hiyo yanalenga katika kukabiliana na swali hilo la Kaini linalotuhangaisha kila siku! Hivyo ili kuonesha shukrani kwa moyo wa kimisionari kwa Mungu Baba, ni vema tukafanya maamuzi ya kubadilisha maisha yetu katika Kwaresima wa mwaka huu 2018. Masomo hayo yana na dhamira husika kuu kama ifuatavyo:
- Toba ya kumrudia Mungu ni kwa njia ya kuondoa aina yoyote ya uonevu na kutenda haki
- Kukiri kuwa tu wakosefu, na tunahitaji kufanya toba.
- Kupatanishwa na Mungu kama watumishi wake ni kuwa tayari kwa lolote hata kama ni kuchekwa au kuhangaishwa na ulimwengu
- Sala, kufunga na kutoa sadaka vifanyike bila ‘kujipigia debe’!
Maamuzi na Utekelezaji ngazi ya Parokia na Jumuiya
Hivyo basi katika kujibu swali ‘Nimrudishie nini Bwana?’, maswali yafuatayo yanapendekeza kitu gani kifanyike:
4.1 Neno la Mungu linasema nini kwa Jumuiya na Parokia yetu kuhusu:
- Toba na thamani ya uhai wa watoto wetu, vijana wetu na familia zetu?
- Toba na haki za binadamu katika mila, desturi, siasa, sheria na uchumi?
- Kama wadhambi tuna wajibu gani mbele ya Mungu na mbele ya binadamu wenzetu?
4.2 Jumuiya na Parokia yetu inaweza kufanya nini ili kurekebisha na kukuza:
- Moyo na tabia ya usikivu kwa sauti ya Mungu anayetuuliza kuhusu hali ya bindamu kama ndugu zetu?
- Moyo na tabia ya kujali utu, hadhi na haki za binadamu wenzetu, hasa wanyonge na wanaogandamizwa?
- Kuchangia katika mabadiliko ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ili maendeleo ya kweli yapatikane kadiri ya tunu za Ufalme wa Mungu?
HITIMISHO
Tukiwa tunaaadhimisha miaka 150 ya umisionari na uinjilishaji nchini Tanzania, tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa upendo wake usiokuwa na mpaka, si tu kwa kumtoa Mwanae wa pekee awe Mkombozi wetu, lakini pia kwa Mwanae mpendwa kuwa sababu ya kumfahamu Mungu. Hivyo basi, tunapofanya adhimisho hili kubwa la Kristo kati yetu, ni fursa ya kumrudia Mungu kwa moyo wa shukrani. Sisi tulioujua upendo wa Kristo, sisi tunaoonja katika maisha yetu nguvu na uzuri wa imani ya Kikristo hatuna budi kumshukuru Mungu. “Nimrudishie Bwana nini kwa Ukarimu wake wote. Nitakipokea kikombe cha wokovu na kulitangaza jina la Bwana” (Zab 116:12). Shukrani ya kweli inadhihirika katika kuwa tayari wa kukipokea kikombe cha wokovu na kulitangaza jina la Bwana. Kwa maneno mengine, huu ni mwaliko wa kuwa “katika hali ya umisionari daima” (EG, 25), unaopingana kabisa na swali alilodiriki Kaini kumuuliza Mungu, ‘Mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?’
Tofauti kabisa na swali hilo la Kaini, ushuhuda wa imani unadai ujasiri na unabii, kama walivyo wale wamisionari waliotuletea imani. Pale tulipolegelega tunapaswa “tuvumbue tena upya na kuongeza shauku yetu ile furaha ya kuinjilisha yenye kuburudisha na kufariji, hata pale ambapo tunapaswa kupanda kwa machozi” (EG, 10).Baada ya miaka 150, uinjilishaji bado upo na unahitajika. Wewe Mkristo, unaitikiaaje? Kwa michango na sadaka zetu zinazofanikisha waseminari kusoma na kuwa mapadri, watawa kupata mahitaji yao, wagonjwa kupewa neno la upendo na faraja, wafungwa kutembelewa, mayatima na wajane kupewa haki zao. Watu kuhudumiwa vizuri katika vituo vya kazi na huduma, hata kuiona sura ya Mungu kupitia sisi, huo ndio uinjilishaji mpya na wa sasa. Katika kipindi hiki cha Kwaresima, ni muhimu kutafakari ni kwa namna gani tunamuishi Kristo, na kwa namna gani tunashindwa kumuishi Kristo na kuomba neema na msamaha wake. Tunahitaji kutambua ya kwamba sisi sote tu wamisionari wa Kristo, kwa wenzetu wapate kumjua kama ambavyo kwa sadaka za watu wengine sisi nasi tulipata kumjua Yesu.
Ni rahisi zaidi kuona kama si kitu sana kuwa Mkristo Mkatoliki kwakuwa tu ndani na tunabahati hiyo. Hatuoni kama bahati tena wala ajabu ya upendo wa Mungu kwetu. Lakini kuna watu wengi sana wanaotamani kumjua Kristo na hawajapata nafasi hiyo, na wengine wanaipata ilihali jua limekwisha kutua. Katika kipindi hiki cha Toba, tukae chini tena na kutafakari kwa upya, ni kwa namna gani maisha yetu yanamuishi Kristo, na tudhamirie kujirudi na kutaka kufanya mapenzi ya Mungu. Hivyo basi, Wapendwa Familia ya Mungu, Kwa moyo wa upendo na kuwajali tunawahimiza waamini mfanye toba ya kweli ili Mungu aguse na abadilishe mioyo yetu, ya raia wengine na viongozi wa nchi. Tuichukulie Kwaresima ya mwaka huu (2018) kuwa ni sehemu ya maandalizi ya adhimisho la Jubilee lenye lengo la kujenga upya Kanisa Katoliki Tanzania na lenye wamisionari wengi watakaoweza kutumwa popote ulimwenguni. Na, mwisho tunapenda kuwatia moyo zaidi ili mshiriki zaidi katika katika maswala ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, na kwa ukristo wenu muwe chumvi na mwanga kwa wote.
Kristo Mfufuka awape amani!
Ni sisi Maaskofu wenu,
1 Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Iringa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
2. Mhashamu Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya, Ofm Cap, Dodoma,
Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
3 Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Dar es Salaam
4. Mhashamu Askofu Mkuu Mstaafu Josaphat Lebulu, Arusha
5. Mhashamu Askofu Mkuu Paul Ruzoka, Tabora
6. Mhashamu Askofu Mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi, Ofm Cap,Mwanza
7. Mhashamu Askofu Mkuu Damian Dallu – Songea
8. Mhashamu Askofu Telesphor Mkude, Morogoro
9. Mhashamu Askofu Bruno Ngonyani, Lindi
10 Mhashamu Askofu Severine NiweMugizi, Rulenge-Ngara
11. Mhashamu Askofu Evaristo Chengula, IMC, Mbeya
12. Mhashamu Askofu Augustino Shao, CSSp, Zanzibar
13. Mhashamu Askofu Damian Kyaruzi, Sumbawanga
14. Mhashamu Askofu Agapiti Ndorobo, Mahenge
15. Mhashamu Askofu Anthony Banzi, Tanga
16. Mhashamu Askofu Desiderius Rwoma, Bukoba
17. Mhashamu Askofu Msaidizi Method Kilaini, Bukoba
18. Mhashamu Askofu Alfred Leonard Maluma, Njombe
19. Mhashamu Askofu Ludovick Minde, ALCP/OSS, Kahama
20. Mhashamu Askofu Castor Paul Msemwa, Tunduru-Masasi (Marehemu)
21. Mhashamu Askofu Michael Msonganzila, Musoma
22. Mhashamu Askofu Mkuu Issac Amani, Jimbo kuu la Arusha
23. Mhashamu Askofu Almachius Rweyongeza, Kayanga
24. Mhashamu Askofu Rogath Kimaryo, CSSp, Same
25. Mhashamu Askofu Msaidizi Eusebius Nzigilwa, Dar es Salaam
26. Mhashamu Askofu Salutaris Libena, Ifakara
27. Mhashamu Askofu Renatus Nkwande, Bunda
28. Mhashamu Askofu Gervas Nyaisonga, Mpanda
29. Mhashamu Askofu Bernadin Mfumbusa, Kondoa
30. Mhashamu Askofu John Ndimbo, Mbinga
31. Mhashamu Askofu Titus Mdoe, Mtwara
32. Mhashamu Askofu Joseph Mlola, ALCP/OSS Kigoma
33. Mashamu Askofu Msaidizi Prosper Lyimo, Arusha
34. Mhashamu Askofu Liberatus Sangu, Shinyanga
35. Mhashamu Askofu Edward Mapunda, Singida
36. Mhashamu Askofu Flavian Kassala, Geita
Comments
Post a Comment