Saudi Arabia yafanya mabadiliko katika nyadhifa za jeshi na wizara

Mfalme Salman wa Saudi Arabia amefanya mabadiliko ya nyadhifa za jeshi na wizara mbalimbali, pamoja na kuteua naibu waziri wa kike akiwa na lengo la kuingiza kizazi kipya serikalini. Sababu za mabadiliko hazijulikani.
Mfalme Salman wa Saudi Arabia ametangaza mabadiliko katika nafasi za juu za kijeshi na wizara mbalimbali nchini humo. Nyadhifa muhimu ya Mkuu wa Wafanyakazi wa Jeshi na za maafisa wengine wa kijeshi zimebadilishwa, wakati vita vikiwa vinaendelea nchini Yemen.
Ufalme wa Saudia haukutoa sababu za kutokea mabadiliko hayo na wala haukutoa maelezo yoyote juu ya namna inavyopanga kuimarisha Wizara yake ya Ulinzi. Katika wakati ambapo Ufalme wake unakosolewa kimataifa kwa kuongoza mashambulizi ya anga nchini Yemen yanayoua raia wa kawaida kwa kulenga masoko, hospitali na maeneo mengine ya raia. Watu wapatao 10,000 wameuawa katika vita hivyo ambavyo Saudi Arabia anaiunga mkono serikali inayotambuliwa kimataifa dhidi ya waasi wa Houthi wanaoudhibiti mji mkuu wa Sanaa kwa sasa. Makundi ya kutoa misaada ya kiutu yanailaumu Saudia kwa kuitumbukiza Yemen katika baa la njaa.
Mabadiliko hayo ya jana Jumatatu yanatazamwa na wengi kama njia ya kuwainua maafisa vijana katika nchi ambayo nusu ya idadi yake ni chini ya umri wa miaka 25. Salman amemteua Luteni wa Kwanza Jenerali Fayyad bin Hamed al-Ruwayli kama mkuu wa wafanyakazi wa jeshi, pamoja na kuteua viongozi wapya katika jeshi la anga na jeshi la ardhini.

Mwanamfalme Mohammed bin Salman
Mfalme huyo wa Saudia pia ameteua manaibu waziri wapya kadhaa, mmoja wao ni mwanamke - ikiwa ni uamuzi wa nadra katika ufalme wenye mfumo dume. Tamadur bint Youssef al-Ramah ameteuliwa kama naibu waziri wa kazi. Nchi hiyo iliteua naibu waziri wa kike wa kwanza mnamo mwaka 2009.
Aidha Salman amemteua Mwanamfalme Turki bin Talal kuwa naibu gavana wa Mkoa wa kusini wa Assir. Mwanamfalme huyo ni ndugu wa bilionea Mwanamfalme Al-Waleed bin Talal miongoni mwa wanawafalme, mawaziri na matajiri waliowekwa kizuizini hivi karibuni katika kile serikali ilichikitaja kuwa ni "ufisadi wa watu wenye vyeo".
Mfalme Salman pia ameteua manaibu gavana watatu kutoka familia za kaka zake, hatua inayoangaliwa kuwa ni kuziridhisha familia zilizohisi zimetengwa wakati alipopata ufalme mwaka 2015. Televisheni ya taifa ya Saudi Arabia imeripoti kwamba mfalme Salman anaingiza kizazi kipya cha vijana katika serikali.
Umaarufu wa Mwanamfalme Mohammed bin Salman, mwenye umri wa miaka 32, unaonekana kuwa ndiyo sababu ya kuingizwa kwa vijana katika serikali yenye misimamo mikali ya kihafidhina.
Mwanamfalme huyo ameanzisha mkakati mkubwa wa mageuzi nchini humo uliopewa jina la Dira 2030, katika jitihada za kuupanua uchumi wa nchi hiyo ili usitegeme uzalishaji wa mafuta pekee, na kuvutia uwekezaji wa kigeni.

Comments

Popular posts from this blog

DOWNLOAD NA USIKILIZE NYIMBO ZA KWARESIMA