GOODBYE AKWILINA
SAFARI njema Akwilina, kwaheri, tangulia mtoto wetu tutaonana, wanadamu wote njia yatu ni moja.
Hizo ni baadhi ya kauli zilizosikika kutoka kwa maelfu ya waombolezaji, wakiwamo wanafunzi wa vyuo mbalimbali na wananchi wa Dar es Salaam, waliojitokeza kuaga mwili wa Akwilina Akwilini (22).
Akwilina alikuwa mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), aliyeuawa Februari 16, mwaka huu kwa kupigwa kichwani na kitu kinachodhaniwa ni risasi, inayodaiwa kufyatuliwa na askari aliyekuwa akitawanya maandamano ya wafuasi wa Chadema.
Jana maelfu ya waombolezaji walijitokeza kuaga mwili wa Akwilina, huku baadhi walishindwa kujizuia na kuzimia wakati mwili ukiingia katika uwanja wa chuo cha NIT ukitokea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ulikokuwa umeifadhiwa.
Pia wengine waliokosa nafasi ya kutoa maneno yao kwa kuzungumza mbele ya umati huo, walionekana kubeba mabango yaliyoshinikiza Serikali kufanya utafiti ili haki itendeke na waliokatisha maisha ya Akwilina aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza chuoni hapo wawajibishwe.
Akwilina anayetarajiwa kuzikwa leo Rombo mkoani Kilimanjaro, hakuwa mmoja wa wafuasi wa Chadema waliokuwa wakiandamana, bali alikuwa abiria katika daladala akipeleka barua ya kuomba kufanya mafunzo kwa vitendo wakati wa likizo yake.
HALI ILIVYOKUWA
Saa 5:30 asubuhi, familia ya Akwilina wakiongozwa na waombolezaji wengine, waliuchukua mwili Muhimbili na kuanza safari ya kwenda NIT.
Msafara uliongozwa na polisi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni.
Wakati msafara huo ukitokea Muhimbili, mamia ya wananchi walionekana kusimama pembezoni mwa barabara ili kushuhudia mwili wa Akwilina ambao ulikuwa umebebwa katika gari maalumu.
Msafara huo uliingia katika viwanja vya Chuo cha NIT, saa 6:30 mchana na kupokewa na viongozi mbalimbali wa vyama na Serikali, kabla ya misa kuanza na baadaye watu kupewa fursa ya kutoa heshima za mwisho kwa marehemu.
Hata hivyo, kutokana na idadi kubwa ya watu kujitokeza na ufinyu wa muda, wengine walizuiwa kuaga mwili huo kuruhusu safari ya kuelekea Kilimanjaro kuanza.
PADRI ATOA NENO ZITO
Misa ya kuaga mwili wa marehemu iliongozwa na Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Yohane, Raymond Manyanga, ambaye alisema mtu aliyefytua risasi iliyomuua Akwilina, anapaswa kwenda kwenye vyombo vya habari na kutubu.
“Inasemekana ni risasi liyomuua Akwilina, risasi haiwezi kwenda yenyewe, imepigwa na mtu… Naamini ni mtu mwenye akili timamu. Nilijiuliza sasa kwanini alipiga risasi, ni jambo ambalo kila mmoja wetu anajiuliza.
“Tumwombe Mungu atupe hekima, busara na kuvumiliana na atuonyeshe hekima ili lisiweze kutokea tukio jingine kama hili,” alisema Padri Manyanga.
Alisema Watanzania wametimiza miaka 50 ya uhuru, hivyo kama nchi haitegemewi kuona matukio ya namna hiyo yakiendelea.
Kwamba Watanzania wanapaswa kuishi kama watu waliokomaa ili kuidhihirishia dunia wamekomaa na kuishi kwa umoja.
“Tusichezee uhai kwa sababu hakuna mwenye uwezo wa kuurudisha, kama ungekuwa unanunuliwa, tungechanga wote na kwenda kununua ili Akwilina arudi, lakini hatuna uwezo huo, tumwombe Mungu, atupe heri kwa sababu hata kama muuaji akifungwa miaka 30, Akwilina hawezi kurudi,” alisema.
Aliongeza: “Tusipopatana tutamalizana, tusipokubali kwamba sisi wote ni watoto wa Mungu. Mtu wa kutuunganisha ni Serikali pekee, kwa sababu ndiyo waliopewa dhamana ya maisha yetu, tunapaswa kumwomba Mungu atusimamie kwa sababu uhai ni zawadi kutoka kwake.”
Alivitaka vyombo vinavyosimamia uchunguzi kuharakisha, ili mhusika aweze kujulikana na kwenda kwenye vyombo vya habari kuomba msamaha.
FAMILIA
Kwa upande wake, msemaji wa familia, Aloyce Shirima, alisema wamesikitishwa na tukio hilo na kuitaka Serikali kuharakisha uchunguzi wahusika waweze kujulikana na kuchukua hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Alisema katika uhai wake, marehemu alikuwa mpole na mnyenyekevu na mwenye kupenda masomo, lakini ndoto zake zimezimwa na risasi iliyosababisha kifo chake.
Shirima alisema kutokana na hali hiyo, ameitaka Serikali kumchukulia hatua kali mhusika wa tukio hilo hata kama ana cheo, ili iwe fundisho kwa wengine.
MABANGO YAIBUKA
Wakati Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Ndalichako, alipopanda jukwaani kutoa salamu za rambirambi kwa waombolezaji waliofika eneo hilo, baadhi ya wanafunzi walionyesha mabango yenye ujumbe mbalimbali kufikisha salamu zao serikalini.
Baadhi ya ujumbe wa mabango hayo ulisomeka: “We are tired of being killed”, “Mwigulu, Siro kwa mauaji haya bado mpo ofisini”, “Wauaji hawawezi kujichunguza wenyewe”.
Licha ya kuwapo kwa mabango hayo, Profesa Ndalichako aliendelea kutoa salamu za rambirambi kwa waombolezaji hao na kusema kuwa Rais Dk. John Magufuli amesikitishwa na kitendo hicho na kuvitaka vyombo vya uchunguzi kuharakisha taarifa za kifo cha Akwilina.
Alisema licha ya rais kutoa kauli hiyo, lakini pia ameomba uchunguzi utolewe haraka iwezekanavyo ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua.
MAKONDA ATOA NENO
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amewataka wananchi wasimnyooshoe kidole mtu yeyote kwa sababu suala hilo linafanyiwa uchunguzi.
“Hatuwezi kuzuia kifo, lakini kwa tendo lililopelekea ndugu yetu Akwilina kuondoka, ndiyo linaacha maswali na leo tumekusanyika hapa, namshukuru Paroko kwa kutukumbusha kuwa wapatanishi na kutuhimiza kulinda amani kwa sababu ni jukumu la kila mwananchi,” alisema Makonda.
MKUU WA CHUO
Mkuu wa chuo hicho, Profesa Zakaria Mganilwa, alisema kuwa kabla ya kifo chake, Akwilina alikuwa miongoni mwa wanafunzi ambao walikuwa ametoka kufanya mitihani ya ‘semester’ ya kwanza.
Alisema katika mitihani aliweza kufanya miwili na kubakisha miwili, huku akichukua barua ya kwenda Bagamoyo kufanya mafunzo ya vitendo (field).
“Akwilina alitoka kufanya mitihani miwili ya ‘semester’ ya kwanza na alichukua barua na kuwaaga marafiki zake kuwa anakwenda Bagamoyo kupeleka barua ya ‘field’, lakini kabla ya kufika umauti umemkuta,” alisema Profesa Mganilwa.
JUMUIYA YA WANAFUNZI NIT
Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha NIT, Mchinja Othuman, alisema tukio hilo limewasikitisha sana na kuiomba Serikali kuharakisha uchunguzi ili wahusika waweze kujulikana.
Alisema polisi wanapaswa kuhakikisha kuwa haki inatendeka katika suala hilo ili kuepusha malalamiko kutoka kwa wananchi.
“Jumuiya ya wana NIT tumeondokewa na mwanadada mcheshi, mpole na anayejituma, naliomba Jeshi la Polisi kuhakikisha haki inatendeka kwa wahusika, hatua kali zichukuliwe juu yao,” alisema Mchinja.
Mara baada ya kumalizika kwa salamu za rambirambi, baadhi ya waombolezaji walipata fursa ya kuaga mwili wa marehemu.
Ni katika hatua hiyo, baadhi ya wanafunzi walianguka na kuzimia.
Hata hivyo, uongozi wa chuo uliomba gari ya huduma ya kwanza kuwapo eneo hilo kutoa huduma kwa wale waliokuwa wanaanguka na kuzimia.
FAMILIA YACHANGISHA NAULI
Licha ya Serikali kutoa magari matatu na moja la kubeba mwili wa marehemu, lakini familia ilitangaza uwepo wa mabasi mengine kwa wananchi wanaotaka kwenda Moshi kwa maziko kuchangia Sh 40,000 kwenda na kurudi.
Katika eneo hilo, wananchi walitangaziwa kuwa kila anayetaka kwenda anapaswa kujiorodhesha kwa wahusika na kulipa kiasi hicho cha fedha.
WASIFU WAKE
Akwilina alizaliwa Aprili mosi, 1996 katika Kijiji cha Holele kilichopo Marangu mkoani Kilimanjaro.
Ni mtoto wa sita kati ya wanane wa familia ya mzee Akwilini na alipata elimu ya msingi katika Shule ya Kitongolia iliyopo kijijini hapo na baadaye kujiunga na elimu ya sekondari katika Shule ya Highland iliyopo mkoani Iringa mwaka 2011 hadi 2014.
Mara baada ya kumaliza kidato cha nne, alijiunga na kidato cha tano na sita na baadaye kujiunga NIT Oktoba 30, 2017 akichukua masomo ya ugavi hadi kifo kilipompata.
Viongozi wengine waliohudhuria mahali hapo ni pamoja na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika.
WAKAZI MKWAJUNI WANENA
Baadhi ya wakazi wa eneo la Mkwajuni, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, ambako ndipo waandamanaji walipotawanywa na Akwilina kuuawa, jana kwa nyakati tofauti walisema vurugu hizo zilisababisha baadhi yao kuishia mikononi mwa polisi licha ya kuwa hawakuwa waandamanaji.
Mmoja wa wananchi hao, Rashid Mrope, ambaye ni fundi wa vitanda, alisema miongoni mwa waliokamatwa ni kijana anayejifunza ufundi ofisini kwake aliyemtaja kwa jina moja la Shabani.
“Baada ya kuanza kurusha juu risasi, watu walianza kukimbia ovyo na kuna kiongozi mmoja aliingia kwenye ofisi ile (akionesha ofisi hiyo) na kujificha nyuma ya meza akavua shati, walipoingia hawakumwona wakawakamata wale waliokuwa pale mwanzoni.
“Hata Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe) anakimbizwa na wafuasi wake kuelekea ofisi za CCM tulishuhudia,” alisema Mrope.
Msimamzi wa mtoto huyo ambaye hakuwa tayari jina lake kuandikwa gazetini, alisema licha ya kuwa ni mdogo pia ni mgeni hivyo hata akiachiwa hawezi kujua aelekee wapi.
Naye Mariam Said ambaye duka na kabati lake la biashara vilivunjwa vioo wakati wa mkasa huo, alisema: “Naona machungu hata kuelezea kilichotokea kwa sababu nimepata hasara na hakuna wa kulipa vitu vilivyoharibika, inabaki kuwa hasara kwangu.”
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwinjuma, Anandume Mwanga, alisema ni mtu mmoja tu aliyefika ofisini kwake kuomba barua ya kumdhamini ndugu yake aliyekamatwa katika maandamano hayo.
“Kaka yake huyo aliyekamatwa alisema ndugu yake alikwenda kutafuta sigara, lakini hakurudi, baadae akapata taarifa kuwa amekamatwa, sijafahamu kama ametoka kwa sababu sijafuatilia. Huyo mmoja ndiye nina taarifa zake,” alisema Mwanga.
Comments
Post a Comment