Boni: Kenya yaanza kuangusha mabomu ‘msitu wa al-Shabab’
Kenya imetangaza kwamba imeanza
kutekeleza mashambulio ya kutoka angani katika msitu wa Boni karibu na
mpaka wa nchi hiyo na Somalia.
Wenyeji wanaoishi msituni wanahamishwa hadi kwenye kambi zilizotengwa na serikali kabla ya mabomu kurushwa.Wanamgambo wa al-Shabaab wanadaiwa kugeuza msitu huo kuwa makao na ngome yao.
Wanamgambo hao wanadaiwa kutumia msitu huo kutekeleza mashambulio katika maeneo ya karibu.
Wiki iliyopita, watu 9 waliuawa kwa kukatwa shingo na wapiganaji hao katika kijiji cha Pandanguo kilicho karibu na msitu huo katika kaunti ya Lamu.
Jumamosi, serikali ilirejesha tena amri ya kutotoka nje usiku katika maeneo ya pwani na kaskazini mashariki mwa Kenya ambayo yameshuhudia mashambulio ya kigaidi kutoka kwa al-Shabab.
Mwandishi wa BBC Ferdinand Omondi anasema wanajeshi wa Kenya wamejaribu kuwafurusha wanamgambo hao kutoka msitu wa Boni kwa miaka miwili bila mafanikio.
Kamishna wa kanda ya Pwani Nelson Marwa, ambaye ametangaza kuanza kwa mashambulio hayo ya angani, amewataka wakazi kukaa mbali na msitu huo kwa sasa.
"Haijalishi mtasema nini, operesheni lazima iendelee. Al-Shabab watafurushwa kutoka msitu huo. Ninavyosema nanyi sasa hivi mashambulio ya angani yanaendelea," amesema Bw Marwa.
"Mambo yatakuwa mabaya sana. Kwa hivyo tunawaomba wale wanaoishi msituni, wahame. Serikali inawahamisha kwa sababu tutafanya operesheni kali kabisa na hatutaki raia wauawe."
Mauaji ya wiki iliyopita yalifufua kumbukumbu za mwaka 2014 al-Shabab walipoua watu karibu 60 katika eneo la Mpeketoni.
Tangu wakati huo, wanamgambo hao wamekuwa wakishambulio vituo vya polisi na kutega vilipuzi barabarani.
Baada ya kushambulia, huwa wanadaiwa kukimbilia msituni.
Comments
Post a Comment