Antonio Rudiger: Chelsea wamnunua beki kutoka Ujerumani


Antonio Rudiger alisaidia Ujerumani kushinda Kombe la Mabara mwaka 2017 nchini Urusi
 Antonio Rudiger alisaidia Ujerumani kushinda Kombe la Mabara mwaka 2017 nchini Urusi 

Mabingwa wa Ligi Kuu ya England Chelsea wamemnunua beki Mjerumani Antonio Rudiger kutoka klabu ya AS Roma kwa mkataba wa miaka mitano kwa £29m.
Rudiger, 24, alikamilisha uhamisho wake wiki moja baada ya kusaidia mabingwa wa dunia Ujerumani kushinda Kombe la Mabara.
"Ni jambo linalonifurahisha sana kwa sababu si kila mchezaji anayepata fursa ya kujiunga na klabu kubwa kama hii," alisema Rudiger.
Ada waliyolipa Chelsea inaweza ikapanda na kufikia £33.3m ukiongeza vikolezo vilivyo kwenye mkataba wake.
"Antonio bado ana umri mdogo lakini ana uzoefu katika ngazi ya klabu na kimataifa na ana sifa zote ambazo zinahitajika kufana katika Ligi ya Premia," mkurugenzi wa kiufundi wa Chelsea Michael Emenalo alisema.
"Ni mchezaji ambaye uwezo wake umethibitishwa."
  • Rudiger atavalia jezi nambari mbili ambayo iliachwa wazi baada ya Branislav Ivanovic kuhamia Zenit St Petersburg mwezi Februari.
Antonio Rudiger ni nani?
Rudiger alichezea timu ya vijana Borussia Dortmund kabla ya kuhamia Stuttgart mwaka 2011.
Alicheza mara yake ya kwanza Bundesliga Januari 2012 na akacheza mara 66 katika Ligi kuu ya Ujerumani kabla ya kuhamia Roma 2015.
Rudiger alicheza mechi 30 Serie A msimu wa 2015-16 akiwa na Roma na kuwasaidia kumaliza nafasi ya tatu na kisha mechi 26 msimu wa 2016-17 walipomaliza wa pili ligini baada ya Juventus.
Pia alicheza mechi sita Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya 2015-16 aliposaidia Roma kufika hatua ya 16 bora.
Rudiger pia alicheza mechi 17 timu ya taifa ya Ujerumani, ikiwa ni pamoja na wakati wa ushindi wa 1-0 mechi ya kirafiki dhidi ya England mwezi Machi.
Rudiger atatumai kwamba uchezaji wake utamhakikishia nafasi kucheza safu ya ulinzi pamoja na Boateng na Mats Hummels katika Kombe la Dunia 2018.

Comments

Popular posts from this blog

DOWNLOAD NA USIKILIZE NYIMBO ZA KWARESIMA